Sunday, November 27, 2011

HALI HALISI NDANI YA IKULU:RAIS KIKWETE AKUTANA NA WAJUMBE WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)LEO MCHANA..

Rais Jakaya Mrisho Kikwete



RAIS Jakaya Kikwete leo atakutana na ujumbe wa Chadema kujadili mchakato wa utungwaji wa Katiba mpya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano,  Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete atakutana na ujumbe huo leo mchana.

Mkutano huo unafuatia ombi la Chadema la kutaka kuonana na Rais Kikwete kumueleza kasoro zilizopo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ambao tayari umeshapitishwa na Bunge na sasa unasubiri kusainiwa na Rais ili  kuwa sheria.

“Mkutano huo ni mwanzo wa mfululizo wa mikutano mingi ambayo Rais Kikwete ameamua kufanya na viongozi wa vyama vingine vya siasa nchini pamoja na wadau wengine kuhusiana na mchakato wa katiba mpya,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.

Kwa mujibu wa Ikulu, Rais anafanya mikutano hiyo kama sehemu ya maamuzi yake kuhakikisha kuwa mchakato huo unaongozwa na mashauriano mapana zaidi miongoni mwa wadau mbalimbali.

Mchakato wa Katiba mpya nchini utaongozwa na Sheria ya Kurekebisha Katiba Mpya ya mwaka 2011 ambayo muswada wake umepitishwa na wabunge hivi karibuni mjini Dodoma lakini  ulisusiwa na wabunge wa Chadema.

Novemba 22, Chadema iliunda Kamati ndogo ya watu sita kwa ajili ya kwenda kuonana na Rais Kikwete na kuwasilisha madai yake juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, uliopitishwa bungeni wiki  iliyopita.

Siku moja baadaye, Rais Kikwete kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, alikubali kukutana na viongozi wa chama hicho.

Aliagiza yafanyike mawasiliano ili kupanga tarehe mwafaka ya kukutana na viongozi hao wa Chadema na kuzungumza suala hilo.

Kamati hiyo ya Chadema iliundwa na  mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, uliofanyika  jijini Dar es Salaam.

Ililenga  kwenda kujadiliana na Rais kuhusu kile walichoeleza kuwa, upungufu wa muswada huo na kutaka Rais atafakari kama ausaini kuwa sheria au la.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliwataja wajumbe  wa kamati hiyo kuwa ni yeye mwenyewe, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Said Arf na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Said Issa Mohamed.

Wajumbe wengine ni Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lisu, ambaye atakuwa Katibu wa Kamati hiyo wakati wa mkutano huo.

Baadaye wiki iliyopita kamati Kuu ya CCM ilimshauri Rais akutane na vyama vyote vya upinzani badala ya Chadema peke yake lakini ushauri huo ukakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Chadema.

Viongozi wa chadema walisema haiwezekani kuunda ujumbe wa vyama vyote kwa sababu wao waliomba na pia vyama vingine vilishiriki katika mjadala wa muswada huo bungeni ambao wao walikataa kushiriki.

No comments:

Post a Comment