Monday, November 28, 2011

Hali Halisi ya Shigongo: Utajiri wa mawazo, mipango muhimu kwa wajasiriamali

Mtoa mada mkuu katika tamasha la Ujasiriamali la Street University, Eric Shigongo akitoa elimu kwa watu waliohudhuria tamasha hilo jana jijini Arusha.
Mratibu wa tamasha hilo, James Mwang’amba naye akitoa mada katika tamasha hilo jana jijini Arusha.
Na Joseph Ngilisho Arusha
JAMII imetakiwa kutokata tamaa ya maisha na kutoridhika mahala ilipo katika kujiongezea kipato  kwa kuwa   njia pekee ya kuepukana na umaskini wa kujitakia ni kuthubutu.

Akizungumza katika mkutano wa kujikomboa na kujiondoa na umaskini kupitia biashara na ujasiriamali uliofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Erick Shigongo alisema kuwa njia pekee ya kuepukana na umaskini ni jamii kuacha woga  na kujenga uwezo wa kujiamini .

Shigongo aliwaeleza wananchi waliokuwa wamefurika katika uwanja huo kuwa hakuna sababu ya nchi yetu kuendelea kuitwa maskini iwapo wananchi wake wanaukalia utajiri.

Alisema katika mafanikio  yoyote ya dhati ni lazima mtu awe na imani  kwamba anaweza kufanikiwa pasipo kujali mtaji alionao isipokuwa awe tayari kuchukua maamuzi ya kujituma na kutokubali kukata tamaa mapema.

Aidha alisema kuwa yeye binafsi hakuwa na fedha lakini alikuwa na imani ya kubadilika kimaisha hivyo alipata fursa kwa kusoma vitabu mbalimbali na kupata ushauri kwa matajiri mbalimbali na hadi sasa amebadilika kimaisha.

Aliyataja mambo makuu muhimu ambayo jamii inapaswa kuyazingatia kuwa ni pamoja na kutokana tamaa,uamuzi, mipango, malengo, utekelezaji wa mpango, uvumilivu, kutoridhika,kujiamini, kuwa na dhamira ya kweli na kuiga mafanikio ya aliyekutangulia.

Alifafanua kuwa daima mtu anapotaka kupata mafanikio asikate tamaa wala asikubali kushindwa kwa urahisi bali aendelee kujenga tabia ya kujifunza kila kukicha ili apate elimu mbalimbali na kujiongezea ufahamu wa namna atakavyoweza kujikwamua kutoka katika umaskini.

Shigongo ameitaka  jamii kuishi maisha yenye historia ya kukumbukwa kwa mema na maendeleo kutokana na kufanya mambo makubwa ya historia katika maisha kwa kujibidiisha katika shughuli na elimu ya ujasiriamali.

Naye James Mwang’amba ambaye pia alikuwa mtoa mada, alisema ni wakati sasa kwa jamii kujenga wazo katika fahamu zao ili kuanza utendaji katika kujitafutia maendeleo ikiwa ni pamoja na kupata marafiki wenye historia ya maendeleo na kusoma kwa dhati vitabu na magazeti kama changamoto ya kuwatoa katika hatua moja kwenda nyingine ya maendeleo.

Aliongeza kuwa si vyema kuwaogopa matajiri na badala yake yajengwe mahusiano ya nguvu na matabaka hayo tajiri kama changamoto itakayoweza kuinua uwezo wa akili ya kijasiriamali itakayoweza kuinua na kubadilisha hali ya maisha tunayokabiliana nayo.

No comments:

Post a Comment