-Muswada wasomwa mara ya pili
-Wabunge wa Chadema wasusia
-Tundu Lissu awachoma Wazanzibari
HATIMAYE muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ulisomwa kwa mara ya pili bungeni jana, licha ya shinikizo la wanaharakati na hoja ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuupinga.
Hali hiyo ilitimia bungeni baada ya serikali kupitia kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, kuuwasilisha na kusisitiza kwamba wale waliokuwa wanataka muswada huo usiwasilishwe kwa mara ya pili walisahau kuwa kwa kufanya hivyo usingejadiliwa katika mkutano huu unaoendelea mjini Dodoma kwa sasa.
Kabla ya Kombani kuwasilisha muswada huo ambao unakusudia kuweka utaratibu wa kuundwa kwa tume ya kuratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi ya kuundwa kwa katiba mpya, Spika wa Bunge, Anne Makinda, naye alisema wanaopinga kuwasilishwa kwa muswada huo mara ya pili wamesahau kuwa wamekuwa wakiutolea maoni kwa takriban miezi minane tangu uwasilishwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Aprili mwaka huu.
Baada ya Kombani na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Katiba, Pindi Chana, kuwasilisha maoni ya kamati hiyo, msemaji wa kambi ya upinzani kuhusu masuala ya sheria na katiba, Tundu Lissu, aliwasilisha maoni ya kambi hiyo huku akionyesha jinsi muswada huo unavyotoa madaraka makubwa zaidi kwa rais ambaye tayari Katiba ya sasa inampendelea.
Kadhalika, Lissu, alisema hakuna uwiano baina ya Watanganyika na Wazanzibari katika vyombo vya uwakilishi kwani kuna kila ukweli kwamba Zanzibar inapendelewa.
Huku akinukuu kauli mbalimbali za viongozi waliotangulia, alisema sasa ni wakati wa Watanganyika kuamua hatima ya mambo yao bila kuwahusisha Wazanzibari ambao nao wamekwisha kutunga Katiba yao huku wakiwa na Baraza la Wawakilishi linaloshughulika na mambo yao lakini Watanganyika hawaruhusiwi kutia mguu.
Baada ya kupinga vipengele vingi vya muswada huo ikiwa ni pamoja na hatari ya Rais kujaza watu wake kwenye tume ili walinde maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitaka muswada huo usisomwe kwa mara ya pili, ila kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, baada ya Lissu kuwasilisha hoja yake, Spika Makinda, alisema ni maoni ya kambi ya upinzani na kumwita mchangiaji wa kwanza kutoka kwa wabunge wa kawaida, Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), lakini kabla ya kuanza kuzungumza, wabunge wote wa Chadema walisimama na kuanza kutoka nje.
Hali hiyo ilifanya Kilango kusubiri kwa muda, huku akisema “tokeni sisi tujadili Katiba. Wabunge wasiokuwa na nidhamu watoke.”
Kilango alishangaa watu wanaosema kuwa Rais amepewa madaraka makubwa katika muswada huo na kuhoji walitaka madaraka hayo apewe nani.
Naye Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, alisema kuwa ana furaha kwa kuwa kwa mara ya kwanza tangu aingie bungeni mwaka 1995 kilio cha chama chao ni kuandikwa kwa Katiba mpya na anashukuru kimetimia.
Aidha, aliwapiga kijembe wabunge wa Chadema na kusema kwamba kwa kauli zao kama wangeshinda urais Muungano ungekuwa umekwisha kuvunjwa, aliwasifu wananchi kwa uamuzi mzuri wa kupiga kura mwaka 2010.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema anaunga mkono muswada huo kwa kuwa anajua kuwa utawashirikisha wananchi katika kupata Katiba mpya.
Mrema alisema hana mahali pengine pa kuzungumzia isipokuwa ni bungeni na kueleza kuwa alichoahidi wananchi wa Vunjo kwamba atashirikiana na serikali kuwaletea Katiba mpya kinatimia. Naye alitupa vijembe kwa Chadema.
Mjadala wa muswada huo unaendelea leo baada ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi.
No comments:
Post a Comment