KWA muda mrefu nimekuwa nikifiria sababu za Watanzania kupoteza utamaduni wao wa upendo na umoja hadi kufikia hatua ya kuwa watu wa kuandamana na kupambana na vyombo vya dola.
Hivi kweli kwamba, hivi sasa uhusiano wa kijamii miongoni mwa Watanzania umeharibika na kusababisha hali tete katika jamii na taifa letu kwa ujumla? Hivi sasa mtu akiamka anafikiria kupambana na maisha.
Watanzania wengi hasa waliozaliwa miaka ya mwanzoni mwa 1980 kushuka chini, wanashangaa jinsi hali ilivyobadilika katika mfumo wa maisha na uhusiano katika jamii. Zamani maandamano, migomo na mapambano na polisi ilikuwa ndoto na jambo la ajabu na hakuna mtu aliyetarajia wala kufikiria kuandamana.
Enzi hizo ukisikia maandamano ilikuwa ya kuwapokea viongozi wa serikali au maadhimisho ya sikukuu fulani ya kitaifa. Kwa mfano mara kadhaa zilitokea vurugu katika shule za sekondari na vyuoni. Ni kweli polisi waliitwa kutuliza ghasia kwa kupambana na wanafunzi lakini wakati huo huo kilitafutwa kiini cha vurugu hizo ikiwamo kuwatafuta wahusika wa vurugu na maandamano hayo. Walichunguza kwa siri na kweli sababu za mtafaruku huo na waliochangia kwa upande wa wanafunzi na upande wa uongozi na utawala.
Mara nyingi baada ya vurugu kwisha iligundulika kuwa utawala mbovu umesababisha wanafunzi waandamane, zilichukuliwa hatua za kuwaondoa viongozi wa juu hasa wakuu kwa kuwapeleka mahali pengine na kuwashusha vyeo au kuwapangia kazi nyingine zisizohusu kusimamia watu na wanafunzi walipewa adhabu za kinidhamu.
Hatua hizo siku hizi hazipo, wanafunzi wakati wote ndiyo wenye makosa na viongozi ni wasafi na watakatifu ambao matendo yao ni haki tupu. Mbaya zaidi wanaunganishwa na makundi vurugu za kisiasa. Nakumbuka wakati vurugu kubwa zilizotokea shuleni zamani zilisababishwa na chakula kibovu. Wanafunzi walifanya vurugu baada ya kubaini kuwa mkuu wa shule ‘anakata mfuko’ wa kununulia chakula na kuuweka tumboni mwake hivyo kuathiri lishe yao.
Pamoja na hayo hivi sasa maandamano imekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania. Mwezi hauishi bila kusikia vurugu vyuoni, shuleni na mitaani. Ipo ya kisiasa na ile ya kijamii huko mitaani. Sababu ya waandamanaji ni kuadia haki juu ya jambo fulani.
Hivi ni lazima haki idaiwe kwa maandamano na vurugu wakati viongozi na mifumo sahihi ya utawala na sheria ipo? Hasha. Tatizo linaweza kuwa waandamanaji hawana imani tena na viongozi wao. Wanaofanya vurugu wanaona viongozi wao hawawasikilizi au wanapuuzia malalamiko yao wanayowaambia kistaarabu.
Viongozi hawataki kuwasaidia kwa sababu wanajua maslahi yao yatakatika. Viongozi wengi wanafikiria siasa zaidi, tena kwa ajili ya manufaa yao na jamaa zao kuliko mambo mengine ya msingi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na mustakabali wa taifa.
Siasa zinazofanywa kwa kuwatumia watu wenye njaa ni hatari wa sababu ni rahisi kufanya vurugu hasa anapoona viongozi wao na kundi fulani la watu wajanja wanafaidi matunda ya uhuru wa nchi yao. Hii ni changamoto kubwa kwa taifa letu.
Matatizo ya Watanzania sasa siyo siasa bali ni ugumu wa maisha unaowakabili na kuzidi kuongezeka kadiri siku zinavyosonga mbele bila kujua watatokaje. Mfumo maisha ya kila siku kwa Tanzania sasa hivi hakuna ajuaye kesho itakuwaje. Kwa mfano Mtanzania wa kawaida hivi sasa aishiye kijiji na mijini, asiye na kazi au aliye na kazi na mfanyabiashara wa kawaida ya mdogo, siku ikipita na kupata chakula anamshukuru Mungu.
Mtu anaamka asubuhi hajui siku hiyo atakula nini, atapaje maji ya kunywa, kupikia, kuoga na kufulia nguo, atafikaje kazini kwa sababu nauli ni tatizo, atapataje karo kwa watoto wake, atapaje daftari na karatasi, akiungua atatibiwaje. Ni ukweli kwamba kuna watu wanatafuta namna wanavyopata mlo mmoja ili siku ipite.
Hivi karibuni nilikuwa nazungumza na mtu mmoja akasema: “Ndugu Mwaijega mimi hapa nina watoto wanne wote wanasoma sekondari, nafanya kazi niko ngazi ya kati, nahitaji kwenda kazini na kuilisha familia yangu na kuhakikisha kuwa watoto wanakwenda shule. Lakini kwa kweli nakueleza kuwa licha ya kuwa na kibanda (nyumba) changu cha kuishi (hivyo silipi kodi) mshahara wangu unaisha kabla ya tarehe 10 ya mwezi unaofuata tena kwa kujibana. Kuna wakati hata nauli ya kwenda kazini nakosa. Hapa nilipo nimejaa madeni Saccos. Maisha ni magumu...”
Pia nilizungumza na vijana kadhaa wakiwamo wahitimu wa vyuo kikuu, ambao karibu majibu yalifanana. “Hapa tulipo mzee hatujui kinachoendelea wala tunakoelekea, tunaona matajiri tu wakiendelea kuneemeka wakati sisi tunaendelea kupoteza mwelekeo, elimu si lolote kwetu. Hivi enzi za ujana wenu ilikuwa hivi? Fikira mimi hapa sasa hivi eti naisha kwa wazazi wangu, nangoja ugali wao na kila kitu. Halafu uwezo wa wazazi wenyewe ni mdogo, wakati mwingine huwa ‘nakausha’ sili, ni aibu kwa kijana kama mimi kuendelea kukaa kwa wazazi.
Tunajaribu kufanya biashara zinagoma mitaji yenyewe kidogo, kazi hakuna chuo kikuu nini bwana. Nashukuru nimesoma nina ujanja kidogo wa kupata senti kidogo lakini zinanisaidia nini. Uchumi wa nchi yetu wenyewe haueleweki, umekaa mguu pande kulegea kabisa... Ndiyo maana hata dada zetu wanaamua kujiuza na vijana wengi wanajiingiza kwenye kubwia na kufanya biashara ya unga (dawa za kulevya). ..”
Ni kweli kwamba hali ya maisha ni ngumu sana kutokana na uchumi wa nchi yetu kuyumba kwa kiasi kikubwa. Mfumuko wa bei umefika kiwango cha asilimia 17.9 ambacho hakijawahi kufikiwa wakati wowote.
Sasa hivi bei za vitu haidhibitiki tena na shilingi inaendelea kuporomoka. Sasa hivi ukiamka asubuhi na kwenda sokoni au dukani unakuta bidhaa zimepanda mara moja au mbili zidi ya jana jioni. Unashangaa ni nini kinaendelea n a inakatisha tamaa!
Juzi (Novemba 18, mwaka huu) jioni Rais wetu Jakaya Kikwete, akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, alisema kwamba, matatizo ya uchumi , kuanguka kwa thamani ya fedha na kupaa kwa mfumuko wa bei, yameikumba dunia nzima na kwamba, serikali inafanya juhudi kulinusuru taifa na hali hiyo.
Nakubaliana naye kwamba, dunia nzima inahangaika, lakini pengine sisi ni zaidi ya nchi nyingine zikiwamo zile tajiri ambazo hazina rasilimali ghafi za kutosha kama tulizonazo.
Ugumu wa maisha ni zaidi ya umasikini unaotukabili kwa sababu tumekalia utaji kwa kukosa maarifa ya kuziibua na kuzitumia kwa manufaa ya taifa letu. Taifa na jamii tajiri ni ile yenye akiba ya kutosha katika ghala zake kama ilivyo kwa Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi pengine kuliko nchi nyingi duniani zikiwamo zilizoendelea ,lakini haitusaidii na kibaya zaidi wageni ndiyo wanaofaidi kwa kuja kuzichukua kirahisi tena kwa gharama nafuu kwa kushirikiana na viongozi wajanja wachache wanaochumia tumboni badala ya kuwanufaisha wananchi.
Hali ngumu ya maisha inayowakabili Watanzania na hasa vijana inachangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa utulivu katika nchi. Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa mara kadhaa amezungumzia hatari ya taifa hili inayotokana na vijana kukosa ajira akifananisha na bomu la nyukli a linalosubiri kulipuka wakati wowote na madhara yake kuikumba nchi nzima.
Sipendi kuingiza siasa katika hili ila alichozungumza Lowassa katika hali ya sasa na tunakoelekea, kina mantiki na kinagusa ukweli kwa sababu ni hatari kuwa na kundi kubwa la vijana wasio na kazi wanaokaa vijiweni bila kazi.
Ni ukweli kwamba wakati watasema tumechoka kukaa kijiweni bila kazi. Bila shaka kusema hivyo si uchochezi ila ni changamoto ya kuliamsha taifa kutafuta mbinu ya kukabiliana na bomu hilo, kwani kila mwaka vijiwe vinaongeza maelfu ya vijana wasio na kazi wanaotafuta maisha!
Matatizo yetu licha ya kuanguka kwa uchumi duniani kote, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mipango duni, utekelezaji na usimamizi mbovu. Ni kweli tungeweza kuwa na matatizo lakini kwa hali yetu, mtikisiko wetu usingekuwa mkubwa kiasi hiki kama watendaji wetu wangekuwa makini.
Chukua mfano wa Rwanda, nchi ndogo isiyo na rasilimali nyingi kama zetu lakini inapiga mbio kimaendeleo. Kenya ambayo inaongoza Afrika Mashariki kwa uchumi imara, licha ya kutokuwa na rasilimali huku ikikabiliwa na sehemu kubwa ya jangwa eneo la Kaskazini, inaendelea kuishinda Tanzania yenye utajiri wa kila kitu.
Wakenya wanajua nchi yetu ilivyo lakini wanaomba usiku na mchana tuendelee kulala na ikiwezekana waje kuchuma rasilimali zetu. Kwa rasilimali zetu, Tanzania ingekuwa tishio Afrika Mashariki kama viongozi wetu wasingekuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali kama walivyo baadhi yao hivi sasa.
Ukweli ni kwamba, kama watu hawana kazi za kufanya, ni rahisi na vyepesi kukimbilia kwenye maandamano kwa vile inakuwa sehemu ya ajiri hata kama ya kujitolea ili nguvu zao zisikae bure. Tunahitaji njia sahihi kukabiliana na changamoto hii.
No comments:
Post a Comment