Monday, December 12, 2011

Posho zaipasua CCM

UAMUZI  uliotolewa juzi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupinga ongezeko la posho za wabunge, kumezua tafrani ya aina yake kutoka kwa wabunge wa chama hicho.
Juzi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipinga nyongeza za posho kama zilivyotangazwa na Spika wa Bunge na kikawataka wabunge wake kutafakari na kuacha kuzipokea.
Wabunge kadhaa wa CCM wamepinga tamko hilo wakishikilia msimamo wao wa kutaka wapewe nyongeza za posho za vikao kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 kwa madai kuwa sababu zilizotolewa na Spika Anne Makinda ni za msingi.
Hata hivyo, wabunge wengine wameunga mkono tamko la CCM la kupinga posho hizo, wakidai kuwa kama uamuzi huo ungetekelezwa ungeleta matatizo na ubaguzi mkubwa katika jamii.
Wa kwanza kuungana na uamuzi wa CCM ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ambaye alipinga ongezeko la posho hizo kwa kigezo cha ugumu wa maisha kwao.
Badala yake alisema ikiwa malipo ya wabunge na watumishi wengine hayatoshi, suala hilo lizungumzwe na kufikiwa muafaka, na ikiwa kutakuwa na haja ya kuyapandisha yalenge watumishi wote na si wabunge pekee.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Makamba alisema si sahihi posho za vikao kuwepo serikalini na hata kwa wabunge na kwamba suala hilo alianza kulizungumza siku nyingi kabla hata CCM haijatoa kauli yake juzi.
“Si sahihi posho za vikao kuwepo serikalini na kwa wabunge, kwa sababu sisi kama wabunge tunapaswa kusimamia matumizi ya serikali na mashirika ya umma, hivyo tukitaka posho za vikao tutashindwa kuwabana wanaokaa vikao na kulipana mamilioni ya shilingi,” alisema Makamba.
Alihoji kwamba kama mtu analipwa posho ya kujikimu (per diem), mafuta, dereva, matibabu na mshahara kuna haja gani ya kulipwa tena pesa ya vikao?
Alisema anaamini kwamba kuna misingi minne ya malipo yoyote ambayo ni unyeti wa kazi yenyewe, usawa na haki kwenye mfumo wa malipo na katika hili alisema: “Haiwezekani watu wa taasisi moja, mfano wewe editor ukalipwa sh milioni saba na Sub Editor sh 700,000.” 
Mbunge huyo aliutaja msingi mwingine kuwa ni rasilimali zilizopo  na hali halisi ya maisha yaliyopo na akaongeza kuwa kama hali ni ngumu, hakuna budi watumishi hao kugawana kilichopo kulingana na ugumu huo wa maisha na hata yatakapokuwa katika hali nzuri.
Alipoulizwa iwapo aliwahi kupokea posho hiyo mpya alisema “Mi sikuwepo bungeni wiki ya kwanza ya Bunge na hadi naondoka sikuipata na hata wabunge wengine hawakulipwa pia,” alisema.
Alisema kwa ujumla msimamo wake ni kwamba hakuna haja ya posho hizo kuwapo katika mfumo wa malipo, vinginevyo mtu akizungumzia kuhusu matibabu au mshahara atamwelewa.
“Ukiniambia allowance inayohusu kazi yangu sikubaliani nayo, kwamba mtu unafanya kazi Wizara ya Nishati na Madini kisha ukadai posho kwa kukaa kwenye kikao kinachohusu kazi yako,” alisema Makamba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, alieleza kushangazwa na suala hilo kukuzwa na kuuliza mbona watu hawahoji watumishi wa serikali wanaolipwa sh milioni moja kwa siku.
“Hili suala linakuzwa bila sababu, mbona kuna watumishi wa serikali wanalipwa sh milioni moja kwa siku watu hawahoji? Iweje iwe nongwa kwa wabunge. Suala hapa ni posho au siasa?” alihoji.
Hata hivyo, alieleza kuwa mpaka wanamaliza mkutano wa Bunge lililopita hawakuwa wamelipwa posho hiyo mpya na kueleza kusikitiskwa na kitendo cha Spika na Katibu wa Bunge kutofautiana katika suala hilo.
Aidha, alisema jamii inapaswa kujadili matatizo yaliyopo kama ukosefu wa ajira kwa vijana, wakulima kukosa masoko na watu wanaoiba fedha za umma badala ya kushupalia suala hilo ambalo alieleza kuwa linakuzwa bila sababu.
“Kwani kabla ya kuwapo kwa hiyo posho wabunge walikuwa hawaishi? Hapa suala hili limepandikizwa ili kuziba mambo mabaya yanayofanyika. Naamini suala hili lipo kuwachanganya wananchi, kuna watu wanaiba mamilioni mbona hawashupaliwi namna hiyo.
“Suala hili linanichefua na kunikasirisha... wananchi wana shida nyingi, hivi ndiyo vitu vya msingi vya kujadili,” alisema na kueleza kuwa hataki kuzungumzia suala hilo kwa kuwa linamchefua.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo, alipopigiwa simu kuzungumzia suala hilo alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa yupo kwenye vikao.
Naye Spika wa Bunge, Anne Makinda, alipofutwa kuzungumzia suala hilo, simu yake ilipokewa na katibu muhtasi wake ambaye alieleza kuwa Spika yupo kwenye kikao ambacho hakufahamu kitamalizika muda gani.
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge, Dk. Kashilillah alipotafutwa alisema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wabunge, kada maarufu na waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu (jina linahifadhiwa) ameweka wazi kuwa Rais Kikwete alikuwa hajasaini ongezeko hilo la posho kwa wabunge.
Kada huyo alisema huenda Kikwete amekwama kusaini nyongeza hizo kutokana na  malipo makubwa atakayopata mbunge kila mwaka ikiwa ni nje ya mshahara wake na malipo mengine.
“Kama nyongeza hizi zitakubalika, basi mbunge angelipwa jumla ya sh 43,560,000 kwa mwaka kama posho ya vikao na fedha za kujikimu, ikiwa ni mbali ya mshahara na marupurupu mengine anayolipwa.
“Kwa mwaka kuna vikao vinne vyenye jumla ya siku 132, hivyo  kwa ongezeko hilo la posho kwa mwaka mbunge analipwa sh 43,560,000…wanaweza kupata mikopo benki hadi ya sh milioni 300 ambayo watailipa ndani ya miaka mitano, sh milioni 90 za kununua gari na pia hupata posho kwenye vikao vya kamati ambayo ni karibu siku 62 kwa mwaka. Vikao hivyo pekee hulipwa sh milioni 7. 3 mwa mwaka pamoja na malipo wanapotembelea nchi za nje kikazi au hapa nchini,” alisema kada huyo.
Alisema pia mbunge hurudishiwa gharama ya mafuta lita kama 120 anaposafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ama fedha alizotumia akitoa risiti ya mafuta anapotumia gari lake binafsi.
Kada huyo alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda, amejinyakulia mamlaka yasiyokuwa yake kwa kutumia udhaifu wa utawala uliopo.
“Mambo yote ya fedha yako mikononi mwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah na hadi sasa katibu ambaye alikuwa Uingereza wakati Spika anatangaza posho, amesikika na kusisitiza kuwa posho mpya hazina ruksa ya mamlaka,” alisema kada huyo ambaye alieleza kushangazwa na ukimya wa Hazina na Ikulu juu ya suala hilo.
Kada huyo wa CCM alisema kinachoonekana katika sakata hili ni fukuto pana ndani ya CCM na taasisi ya Bunge, hivyo ni vema likaangaliwa kwa mtizamo tofauti badala ya kuliona la kawaida kama masuala mengine.
Katika taarifa ya CCM iliyotolewa juzi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilieleza kuwa suala la kupanda kwa gharama za maisha haliko Dodoma wala kwa wabunge  peke yao, bali ni la nchi nzima na ndiyo maana nyongeza hizo  zimezua mjadala mkubwa  miongoni mwa wananchi wa kawaida, wasomi na wanasiasa walioeleza kuwa nyongeza hizo ni ufujaji wa fedha wakati huu ambapo makundi ya watumishi wengine wamekuwa wakidai kulipwa mafao yao na serikali bila mafanikio.
Desemba 6 mwaka huu, Spika wa Bunge, aliutangazia umma kuwa posho za vikao vya wabunge zilikuwa zimeongezwa kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000  kutokana na kile alichosema kupanda kwa gharama za maisha katika mji wa Dodoma na kwamba wabunge walianza kulipwa katika mkutano wa Bunge uliopita.
Kauli ya Makinda ilipingana na ya Katibu wa Bunge ambaye alieleza kuwa posho hizo hazijaanza kulipwa kwa kuwa lilikuwa ni pendekezo ambalo limepelekwa kwa rais ili aweze kuliidhinisha.

No comments:

Post a Comment