Friday, May 25, 2012

Mgosi aiombea msaada familia ya Mafisango


Mussa Mgosi.
Na Khatimu Naheka
KIUNGO mshambuliaji wa DC Motema Pembe ya DR Congo, Mussa Mgosi, amezitaka klabu za Simba na Azam FC kufikiria juu ya kuisaidia familia ya kiungo wa zamani wa timu hizo, Patrick Mafisango.
Mafisango ambaye alifariki Alhamisi iliyopita aliwahi kuzichezea klabu hizo kwa nyakati tofauti, ambapo katika msimu uliomalizika alikuwa msaada mkubwa katika kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 11 kwenye ligi hiyo.
Akizungumza kutoka mjini Kinshasa, Mgosi aliyewahi kucheza na Mafisango akiwa Simba kabla ya kutimkia DC Motema Pembe amesema kifo cha mchezaji huyo kimeacha hali ngumu kwenye familia yake.
Alisema marehemu ameacha watoto watatu ambao anaamini wanaweza kuwa na wakati mgumu kutokana na hali ya maisha ya DR Congo.
“Huku (DR Congo) maisha ni magumu sana, marehemu ndiye alikuwa kila kitu katika familia yake sasa kifo chake kimefanya familia yake kuwa kwenye hali tata, natoa wito kwa Simba na Azam kuangalia uwezekano wa kuisaidia hii familia kwa chochote,” alisema Mgosi.

No comments:

Post a Comment