KANISA Katoliki nchini limesema haliridhishwi na utaratibu wa unaotumiwa na serikali kulituhumu kanisa hilo kuwa linajihusisha na biashara ya dawa za
kulevywa.
Kanisa limetoa kauli hiyo siku siku chache baada ya semina ya wabunge kuhusu athari za dawa za kulevya nchini iliyofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Semina hiyo ili kuwa ni ahadi ya serikali kutekeleza ahadi iliyoahidi kuhusu kuonesha mkanda wa video wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuonesha hadharani.
Kanisa Katoliki nchini na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) yalikuwa miongoni mwa taasisi za dini ambazo zilitajwa kutumiwa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kufanya biashara ya dawa za kulevya.
Taarifa iliyosainiwa na Katibu wa Baraza la Maaskofu (TEC), Padri Anthony Makunde na kusambazwa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kanisa hilo linaamini kwamba biashara hiyo itakomeshwa iwapo wahusika wote, pasipo kujali wadhifa wao katika jamii, watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria na si kwa malumbano na kauli zenye utata ambazo malengo yake yanatia shaka.
"Tumepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa kwa kuzingatia hadhi na ushawishi ambao kanisa inao mbele ya jamii pamoja na maadili yanayofudishwa na kusimamiwa na taasisi hiyo.
"Habari hizi zimelisikitisha na kulifadhaisha sana Kanisa Katoliki kwa vile, kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari kauli hiyo imetolewa katika semina ambayo sisi kama Taasisi hatukualikwa au kuwepo hivyo kushidwa kutoa maelezo juu ya shauri hili.
Alisema kuwa kanisa hilo limeshangazwa na taarifa hizo kwa sababu halijawahi kudokezwa ama kushirikishwa juu ya suala hilo ili kutoa ufafanuzi na pengine ushirikiano iwapo ungehitajika.
Ni kwa mantiki hiyo, Kanisa Katoliki linasubiri maelezo na taarifa rasmi kutoka mamlaka husika ili liweze kutoa ufafanuzi na pengine ushirikiano iwapo utahitajika.
"Tukio lililotajwa katika magazeti ni Kongamano la Vijana lililofanyika huko Australia 2008. Katika tukio hilo ni kweli kwamba Baraza la Maaskofu liliratibu safari ya vijana na walezi wao waliohudhuria Kongamano hilo. Kwa mujibu wa taarifa zetu, vijana na walezi waliopitia TEC walienda na kurudi wote.
"Hatuna taarifa za vijana waliobaki Australia kutoka katika kundi la vijana ambao safari yao iliratibiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
"Hata hivyo inashangaza kuona kwamba safari iliyofanyika miaka mitatu iliyopita inanukuliwa katika siku hizi katika hali ambayo Kanisa Katoliki halijawahi kuulizwa, au kuamriwa na mamlaka husika kutoa taarifa zozote kuhusu kundi ambalo safari yao ya kwenda Australia iliratibiwa na Kanisa hili ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa hata hivyo mwaka huu kuanzia tarehe 16/8/2011 vijana wa Kitanzania wakiwa na walezi wao walikuwa Madrid- Hispania kwa Kongamano la aina hiyo. Kilele chake kimefanyika Agosti 21 mwaka huu kwa Ibada ya Misa iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Benedicto VI.
"Ikumbukwe kuwa si mara ya kwanza Kanisa Katoliki kuratibu safari za Kiroho na Kichungaji kwa makundi mbali mbali ya waamini wake. Ziko safari za kwenda nchi Takatifu, Roma, Fatima, Lurdi na sehemu nyinginezo za Hija.
"Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limekuwa ikiratibu safari hizo baada ya kujiridhisha kwamba wale wote wanaokwenda kushiriki katika Hija hizo wamefuata taratibu zilizowekwa kikanisa na kuridhika kwamba wanakwenda huko kwa lengo la kuhiji na si vinginevyo.
"Kwa vile si sera ya Kanisa Katoliki kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, Kanisa Katoliki linaamini kwamba hata ikitokea kwamba mmoja wa mahujaji amebainika kujihusisha na biashara hiyo, atakuwa amefanya hivyo kama mtu binafsi na si kwa jina ama kwa niaba ya Kanisa.
"Kanisa linaunga mkono harakati zote za serikali na watu wote wenye mapenzi mema za kupiga vita biashara hiyo haramu. Hata hivyo taarifa ilisema kanisa halitaunga mkono kauli za jumla jumla zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu dawa za kulevya ambazo pengine zinatia shaka iwapo lengo lake ni kweli kupiga vita dawa za kulevya ama kulichafua, kulidhalilisha na kulipotezea hadhi na mvuto lililonao mbele ya jamii
No comments:
Post a Comment