MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge wiki iliyopita, umeendelea kupingwa baada ya asasi za kiraia 180 kuitisha maandamano ya nchi nzima, ili kumsihi Rais Jakaya Kikwete asiusaini kuwa sheria kamili kwa sababu msingi wake ulikosewa.
Akitoa tamko kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini Muswada huo umekosa sifa za kuufanya kuwa sheria.
“Tunaandamana ili kumsihi Rais Kikwete asisaini Muswada huu kwa sababu msingi wake ulikosewa na kukosa sifa ambazo zinatakiwa, sisi tupo asasi za kiraia 180, wote tumekubaliana katika hili,” alisema Kibamba.
Alisema maandamano hayo yatafanyika Jumamosi ijayo na yataanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
“Tumekubaliana maandamano haya yataanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia Viwanja vya Jangwani, lakini pia maandamano kama haya yatafanyika kila mkoa na wilaya za nchi hii,” alisema Kibamba.
Alisema wameamua kutumia maandamano ili kuonyesha kitendo kilichofanywa na Bunge kupitisha Muswada huo kilikuwa ni sawa na hujuma kwa wananchi.
Alisema, wabunge walikosa fursa ya kujadili Muswada huo kwa maslahi ya wananchi, badala yake walijikita katika mambo yasiyokuwa na tija, ikiwemo jazba na mipasho ya kusema watu, huku wakionyesha nani anajua kumsema mwenzake zaidi.
“Mchakato huo umeingilia uhuru wa wananchi, wabunge walikosa fursa ya kuujadili, kwani badala ya Muswada walijadili watu kwa jaziba, mipasho na kubeza wananchi, ni dhahiri wabunge hao wamebeba ‘jinai’ dhidi ya wananchi.
“Na hii maana yake ni kwamba kadri wanavyopeleka mambo haya kienyeji na kiujanjaujanja, kuna hatari ya Rasimu ya Katiba kukataliwa na wananchi huko mbele ya safari… sisi hatutaki tufike huko maana yatakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania kuandaa kitu ambacho mwisho wake kitakataliwa.
“Tunaandaa maandamano haya ili kumsihi na kumshauri Rais asiweke saini, kwa sababu tunajua anayo mamlaka kikatiba kutotia saini Muswada huo, ili urudishwe bungeni na wananchi wapate fursa waliyonyimwa, na hii itamjengea heshima kwa mara ya pili, baada ya ile ya kwanza ya kukubali kuipa Tanzania Katiba mpya ili kuepusha taifa kuingia katika mgongano na migogoro isiyo na tija.
“Msimamo wa Jukwaa ni kwamba, mjadala wa Muswada huo haujahitimishwa na tulaani maelezo yasiyokuwa na ukweli yaliyotolewa na wabunge wakati wa kujadili mchakato huo, tunasisitiza haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili, kwa sababu haukutoa fursa adhim na muhimu kwa wananchi kuujadili,” alisema Kibamba.
Alisema Muswada huo, haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kabla ya kufikishwa kwa wananchi vijijini na mijini, Tanzania Bara na Zanzibar, ikizingatiwa kuwa ndiyo kwanza ulikuwa umeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza.
“Wabunge walipaswa kujiuliza, je, nyumba ikijengwa juu ya msingi dhaifu itaweza kudumu, Muswada wa Katiba ambao hauna ridhaa ya wananchi utakuwa unatengeneza Katiba ya nani na kwa faida ya nani.
“Jukwaa la Katiba linaamini kuwa mchakato ambao haukushirikisha wananchi kutoka hatua ya awali ya utengenezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba hauwezi kuwa na manufaa kwao,” alisema.
Wabunge wanawake CCM lawamani
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza bungeni kujadili Muswada huo, wameshutumiwa vikali na wanawake wenzao, wakisema hawakuwatendea haki wanawake masikini walioko pembezoni kwa kukubali kupitisha muswada huo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya, alisema amesikitishwa na kauli za mipasho zilizoonyeshwa na wanawake hao, ilhali ameshiriki kwa namna moja au nyingine kuhakikisha wanawake wengi wanaingia katika vyombo vya maamuzi kama Bunge ili kutetea maslahi ya watu masikini, hasa wanawake.
“Naomba niseme ukweli wangu leo (jana), nimesikitishwa, sikutegemea wanawake niliowapigania binafsi kuingia katika vyombo vya maamuzi kama hivyo, hawa wangesimama na kukataa kile kinachotaka kutengenezwa ni batili kwa watu masikini.
“Matokeo yake tulishuhudia mipasho na kebehi, najiuliza mara mbili kama niendelee kutetea tena wanawake wa jinsi hii ama la, kama wanawake wenzetu walio katika Bunge wamewaangushwa Watanzania, wametuangusha wanawake wenzao, hili limeniuma sana.
“Kwa kutambua umuhimu wa Katiba yenye ‘ownership ya wananchi,’ hasa makundi mbalimbali ya kijamii na kwa kutambua Katiba ndiyo inabeba maadili ya kitaifa, hii ni sheria kuu, ndiyo maana tunaipigania na siyo kitu kingine.
“Wasije wakafikiri tunataka hizo siasa zao, sijawahi kutamani siasa, hatutaki hivyo vyeo vyao, kwa sababu huku niliko naweza kutetea wananchi kwa mapana bila vikwazo,” alibainisha Nkya.
Kibali cha Polisi
Walipoulizwa kuhusu maandamano yao kama yameruhusiwa na Jeshi la Polisi, Kibamba alisema dhana ya kibali ni tafsiri potofu ya Katiba ya nchi.
Alisema Ibara ya 12-18 ya Katiba, kuhusu tamko la haki za binadamu, inaeleza wazi kuwa kila raia wa Tanzania, ana haki ya kutoa maoni pamoja na kukusanyika mahali popote.
“Sisi tumefanya mawasiliano na Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kuhusu maandamano ya nchi nzima, na katika hili nawasihi polisi waheshimu Katiba hii kwa sababu bado tunaitumia hadi hapo tutakapokuwa tumepata nyingine.
“Tuko tayari kukutana na makamanda waliosomea masuala ya intelijensia, tuwaeleze, hatutaki hata ukucha wa mtu uumie, lakini pia tunaomba bendi ya Jeshi la Polisi ije kutusindikiza, tuna uzoefu wa kufanya maandamano ya amani,” alisema Kibamba.
Tunawataka Watanzania wote wajitokeze kwa wingi, polisi wenye dukuduku la maslahi yao waje, lakini wasivae sare kwa sababu wananchi wanaweza kuogopa, lakini makundi mengine kama majaji, maskofu, mashehe, wakitaka waje na sare zao.”
Wiki iliyopita akihutunia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alisema atasaini Muswada huo ifikapo Desemba mosi, ili uanze kutumika rasmi.
Alisema amefikia uamuzi huo, baada ya Bunge kuupitisha kwa kufuata taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya wananchi tofauti na baadhi ya watu wanavyotaka kupotosha umma.
Alisema atashauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, namna ya kuteua wajumbe watakaounda tume ya kuratibu maoni ya wananchi kwa kuzingatia vigezo vyote vinavyotakiwa.
TUCTA NAYO NDANI
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hezron Kaaya, alisema wao kama taasisi kubwa inayobeba wafanyakazi hawakuwahi kushiriki mchakato huo, jambo ambalo limewanyima haki wafanyakazi kuweka msingi tangu awali ambao ndio utapelekea kupatikana Katiba inayokubalika.
“Sisi kama taaisisi kubwa tunaona fahari kuwa pamoja na wenzetu asasi za kiraia kwa sababu wote tunapigania maslahi ya Watanzania na katika hili wafanyakazi nchi nzima watashiriki maandamano haya, ili kumsihi Rais asisaini Muswada huo na akifanya hivyo atakuwa ametambua wajibu wake kwa Umma.
“Hatuamini kama Rais atatupuuza, lakini endapo atatupuuza tutafanya mchakato mbadala wa wananchi, tutaunda chombo maalum cha kusimamia maoni ya wananchi kwa sababu kuna uwezekano mkubwa utaratibu uliotumika kupitisha Muswada huu ndiyo utatumika kupitisha rasmu ya Katiba, iliyopo tunaiheshimu lakini tunataka kuondoa mianya ya uonevu kwa Watanzania,” alisema Kaaya.
No comments:
Post a Comment