Sunday, November 27, 2011

Kishindo CCM


*Nape hatarini kung’olewa uenezi
*JK ajipanga kuvunja makundi, mahasimu
*Wasiwasi watanda, kila mmoja na utabiri yake

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKATI joto la kisiasa likizidi kupanda miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi kwa ujumla, Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kutumia uwiano wa kisiasa (political balancing act), ili kujaribu kurejesha amani ndani ya chama hicho.

Chanzo cha habari ndani ya vikao vya juu vya CCM vinavyoendelea, kimeliambia MTANZANIA kuwa lengo kuu la mkakati huo ni kuhakikisha makundi hasimu yanavunjwa na viongozi wanaotajwa kuwa katika mapambano wanashughulikiwa mmoja mmoja.

Mahasimu wakuu wanaotajwa ndani ya chama hicho ni kundi linalojiita wanachama ‘waadilifu’ na kundi jingine ni ambalo wale ‘waadilifu’ wanaliita la mafisadi.

“Ninachoweza kukwambia  ni kuwa, Mwenyekiti wetu ni lazima avunje makundi yenye uhasama ndani ya chama, kwa sababu bila kuyavunja, basi chama kiwe tayari kuvunjika vipande vipande na hili hatuwezi kukubali litokee.

“Na ili aweze kuvunja makundi hayo hasimu, hana budi kushughulika na wale wanaotajwa kuwa viongozi wa makundi. Sasa hawa watajieleza na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.

“Si sahihi kusema wafukuzwe na katika hili, tunaweza kuamua kutumia busara ya madaktari pale wanapomshauri mgonjwa wa kansa kutokata sehemu yenye mwili iliyoathirika na ugonjwa huo, kwa sababu kwa kuikata mgonjwa baada ya muda mfupi anaweza kupoteza maisha.

“Haya mambo ya kutimuana nadhani wote tunakumbuka yalivyoigharimu Zanzibar, ambapo kwa miaka wakasahau mambo ya msingi ya maendeleo, badala yake wakapoteza muda mwingi kwenye malumbano. Nadhani ni vema kujifunza kutokana na makosa tuliyofanya siku za nyuma,” alisema.

MAHASIMU KUSHUGHULIKIWA
Mahasimu wanaotajwa zaidi katika mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa unakiyumbisha chama ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Vyanzo vya habari vimesema kuwa, chama kinakusudia kuchukua hatua dhidi ya wote wanaotajwa, ambapo miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kumuondoa Nape katika nafasi yake ya sasa.

Katika hatua hiyo, bila kutaja muda halisi wa utekelezaji wake, zimesema kada huyo kijana ambaye anatuhumiwa kuchochea moto wa uhasama, atapangiwa kazi nyingine katika moja ya balozi zetu nje, na nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, ambaye pia kwa nyakati tofauti amekuwa akitoa kauli tata katika mikutano ya hadhara.
“Kumpangia kazi nyingine Nape ni sawa, kwa sababu hata hii dhana ya kujivua gamba ni yeye ambaye awali kabisa aliipotosha, ingawaje sasa anajaribu kufukia mashimo, lakini kumweka Lusinde badala yake itakuwa ni hatua kubwa kuelekea kukiua kabisa chama,” alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.

NAPE ALAMBA MATAPISHI YAKE

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Nape alisema kuwa, dhana ya kujivua gamba kamwe hailengi mtu, lakini lengo lake ni kuleta mageuzi ndani ya chama hicho katika nyanja mbalimbali.

Katika mkutano huo, alivilaumu vyombo vya habari kwa kile alichokiita kutomuelewa na kupotosha ukweli, na kuahidi kuwa, kuanzia sasa chama hicho hakitavumilia tena upotoshwaji unaofanywa na vyombo vya habari.

Kwa wale wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa, watakumbuka kuwa baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kutangaza dhana ya kujivua gamba mjini hapa Februari 5, 2011, Nape na Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Chiligati, walizungumza na vyombo vya habari
.
Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, waliwataja watuhumiwa watatu wa ufisadi ambao ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Lowassa na Chenge na kuwataka ndani ya siku 90 wawe wamejiondoa wenyewe, vinginevyo chama kitawaondoa.
Pia siku ambapo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alipokutana kwa mara ya kwanza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Nape alirudia kauli ya siku 90 na kusababisha kupingana hadharani na bosi wake, ambaye alisema hilo halikuwapo katika ajenda za vikao vya CCM.

Lakini jana katika hali ya kushangaza, Nape hakuzungumzia siku 90 na badala yake alisema mpango au dhana ya kujivua gamba ni suala la muda mrefu.
Alipobanwa zaidi aliseme; “Jamani mtu anapoamua kuoga, ni lazima awe na pa kuanzia, iwe miguuni au kichwani, kujivua gamba ni mageuzi ndani ya chama yatakayochukua muda mrefu.

“Dhana haijaeleweka vizuri, kusimamia uadilifu si kuleta mpasuko ndani ya chama na kutenganisha wabadhirifu na waadilifu si kubomoa chama.”

Nape, aliwalaumu wanaomuhusisha na makundi ndani ya chama, na kudai yeye hana kundi, ila wanaomuhusisha  wanatafuta njia ya kukwepa majukumu.

Alikiri kuwapo kwa hali kubwa ya wasiwasi miongoni mwa wana-CCM na wananchi, na kuvituhumu vyombo vya habari kwa kusababisha hali hiyo, ambapo alisema hali ndani ya vikao vinavyoendelea ni shwari na tulivu.

Lakini taarifa zilizozagaa mjini hapa zinadai kuwa, kauli hizo za Nape zina lengo la kupoteza lengo, ilhali akijua kuwapo kwa mipango na mikakati ya kuwaumiza kisiasa mahasimu wake na wa kundi lake, kabla ya kumalizika kwa vikao mwishoni mwa wiki hii.

Mwisho.

MWAKYEMBE AMPONZA SITTA
*Ahojiwa Polisi kuhusu tuhuma za sumu

Na Mwandishi Wetu

JESHI la Polisi nchini limemhoji Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuhusiana na tuhuma alizotoa akidai mafisadi wamempa sumu Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye yupo nchini India kwa matibabu.

Chanzo cha habari cha kuaminika ndani ya jeshi hilo kimesema, baada ya Sitta kuhojiwa na kutakiwa kuwasilisha ushahidi wa tuhumu alizotoa, alipeleka ushahidi ambao uliwashangaza  wengi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
“Mzee baada ya kutoa zile tuhuma, tuliona si jambo dogo, linaweza hata kuhatarisha amani ya nchi hivyo tukaona ni busara tumhoji, atupatie ushahidi wake, ili sisi kama wanausalama tuufanyie kazi.
“Lakini kilichotuchekesha na kutushangaza, akatuletea ushahidi kutoka kwenye mitandao ya jamii, akijua kabisa ule si ushahidi mbele sheria pamoja na kuwa yeye ni mwanasheria.
“Katika mambo yanayoandikwa kwenye mitandao ya jamii, kuna mengi ya kweli na uongo, ndio sababu hata wachangiaji wengi hawaweki majina wala anwani zao hali, sasa ni vipi mtu anazungumza mambo mazito kwa ushahidi wa aina hiyo?” kilihoji chanzo chetu.
Katika ushahidi huo wa Sitta (nakala tunayo) pia yeye binafsi anatajwa kuwa mmoja wa walengwa katika mkakati wa kuua watu kadhaa.

Wengine waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwanahalisi, Saed Kubenea.
Sitta, ambaye ni rafiki mkubwa na mshirika wa karibu wa Dk. Mwakyembe katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini, alisema wasiwasi huo unatokana na mabadiliko ya ngozi na nywele aliyoondoka nayo nchini kwenda India, ambayo ni mara ya kwanza kuishuhudia katika kipindi chote cha maisha yake.

Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alitoa kauli hiyo katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha ITV katika kipindi chake cha Dakika 45, kilichorushwa hivi karibuni.
“Ijumaa iliyopita nilikwenda kumuona nyumbani kwake, Kunduchi Mtongani. Nilishtuka sana. Kwa sababu umri wangu sasa wa zaidi ya miaka 65, sijaona mtu anajishika halafu inatoka vumbi, inadondoka chini kutoka kwenye ngozi,” alisema Sitta.

Aliongeza: “Kuna kitu kama mba kwenye nywele na kwenye ngozi ya Dk. Mwakyembe. Akishika hivi, baadhi ya nywele zinadondoka. Mkono umevimba, sehemu mbalimbali. Mke wake alichukua video. Alikuwa anatuonyesha kwenye laptop (kompyuta ndogo). Kwa kweli inatisha.”
Alisema inatisha zaidi hasa baada ya madaktari bingwa nchini kushindwa kugundua kitu kilichomsababishia Dk. Mwakyembe kupatwa na hali hiyo, hadi anaondoka kwenda nchini India kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, alisema anamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuamua Dk. Mwakyembe apelekwe India kwa madaktari bingwa, ambako itajulikana nini kilichomsababishia hali hiyo.

“Lakini kilichokuwa kinaonekana dhahiri pale ni uwezekano wa kitu cha hovyo kuwa kimefanywa cha aina labda ya sumu,” alisema Sitta.

Hata hivyo, alisema anamuachia Mungu kwani kila mtu ana siku yake ya kuondoka duniani.

Akijibu swali namna anavyoliona suala la kuugua huko kwa Dk. Mwakyembe, Waziri Sitta alisema ni kama limechukua sura ya kuwekeana sumu na vitisho.

Hata hivyo, alisema suala hilo linabaki kuwa ni sehemu ya mapambano na kukumbusha kila mwanadamu amezaliwa siku moja, hivyo kufa ni lazima.

“Kwa hiyo, sijui mambo haya yamefanywaje. Mimi napata vitisho kwenye simu. Utaona namba zangu za simu nabadili mara kwa mara kwa sababu natishiwa sana. Na vita bayana ipo kwenye magazeti yao,” alisema Waziri Sitta.

Kabla ya Dk. Mwakyembe kwenda India kutibiwa, kulikuwa na habari kwenye magazeti kuwa alikuwa amelishwa sumu, ingawa yeye binafsi hajakanusha waka kuthibitisha habari hizo.

*Katika toleo la MTANZANIA kesho tutachapisha ushahidi huo neno kwa neno.

No comments:

Post a Comment