Sunday, November 27, 2011

Jamanii Hali Halisi ya Kujua kuwa Kikwete rais wa CCM au CHADEMA?

INAWEZEKANA kabisa umoja wa kitaifa ukamomonyolewa na watu wachache wanaoamka kutoka usingizini wakidhani kuwa nafasi ya rais ni ya kichama zaidi kuliko nguvu na mamlaka ya wananchi waliyonayo kisheria katika kumpata kiongozi mkuu wa nchi.
Rais si taasisi ya chama na chama hakina mamlaka ya kumwapisha kiongozi huyo mkuu wa nchi hata kama ametoka ndani ya chama cha siasa kilichopata ushindi,chama ni sawa na reli inayopitisha mabehewa ya treni na abiria ili yaweze kufika kule yanakowapeleka na kuiacha reli ikiwa hapo hapo ilipo.
Ndiyo maana kuna utata mkubwa katika medani za kisheria linapokuja suala la mgombea binafsi na kwa kiasi kikubwa tafsiri za kisheria na haki ya kuwepo kwa mgombea binafsi kumeonekana zaidi kugusa utashi wa chama tawala badala ya kutii matakwa ya kisheria ili kuondoa haya yanayojitokeza leo.
Tabia ya kudhani na kufikiri kuwa urais ni nafasi ya chama kwa vile kumeegemezwa na kasumba ya kuwa na Mwenyekiti huyo huyo anayeitwa kwa kofia nyingine ya urais ndani ya vikao vya chama anachotoka kunazidi kuwapumbaza zaidi wale waliojisahau na kufikiri kinyume wanapoweka masharti mbele ya rais ali asikutane na Watanzania wasiokuwa wana CCM.
Kitendo cha uongozi wa juu wa CCM kumtaka rais Jakaya Kikwete asikutane na watanzania wanaotaka kumuona kutoka chama kingine cha siasa kwa lengo la kuzungumzia mustakabali wa nchi na mchakato wa kupata katiba mpya ni kosa kubwa.
Kosa kubwa ambalo halikutegemewa na Watanzania wengi wenye akili timamu na upeo wa kujua mambo ya mbele kabla hayajatokea ni hii hatua ya Kamati Kuu (CC) ya CCM kutoa masharti ya kushangaza yanayomtaka rais wa nchi akutane viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na wala si wa Cahdema pekee kama chama hicho kikuu cha upinzani kilivyotaka.
Eti Rais Kikwete hatakiwi kuonana na CHADEMA pekee yao na ili viongozi hao wa upinzani waweze kuingia Ikulu lazima waongozane na viongozi wa vyama vingine vya upinzani hapo ndipo watakapopata fursa ya kuongea na rais .
Hoja hii ndiyo inayoanza kuwagawa wananchi na hakukuwa na sababu yoyote ya CCM kama chama cha siasa kikongwe kije na masharti ya kibaguzi dhidi ya chama kingine cha siasa,vyama ambavyo kimsingi vyote vimesajiriwa kwa mujibu wa sheria ya nchi na hakuna chama kilichosajiliwa kutoka Ikulu.
Kama nilivyosema nafasi ya rais inatokana na mamlaka ya umma inatokana na ridhaa ya wananchi wengi bila kuzingatia itikadi ya vyama vya siasa na kwa vyovyote wengi wanaompeleka rais Ikulu idadi yao kubwa si wana CCM ni Watanzania kwa matakwa yao.
Kwa hoja hii ya CCM ya kufikiri kuwa kwa kuwa Kikwete ni mwenyekiti wa taifa wa chama hicho basi hawezi kufanya maamuzi yoyote ya kiserikali hadi hapo chama chake kinaporidhia afanye nini bila kujali kuwa kofia hizo mbili alizozivaa kwa wakati mmoja, moja ya kofia ina madhara makubwa.
Madhara makubwa anayoweza kuyapata Mwenyekiti wa CCM ni yale ya kuidhoofisha serikali yake pale inaposhindwa kusimamia vema sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kutokujali misingi ya haki na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuwa havikuwekwa na wapinzani isipokuwa ni maamuzi ya kisheria ya kuwepo kwa mfumo huo.
Rais anayezingirwa na maamuzi ya kisiasa, akifungamana zaidi na nguvu ya chama anachotoka katika masuala ya kitaifa anapoteza imani kubwa waliyonayo wananchi juu ya mamlaka waliyompa na kusababisha kuzuka kwa tafsiri tofauti zinazohoji kuwa huyu ni rais wa CCM au wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Haiwezekani na haiingii akilini rais wa nchi azuiwe na chama cha siasa tu kwa sababu kilikuwa daraja la kumvusha afike Ikulu anakuwa mali ya chama na mamlaka yake aliyopewa na umma yanamezwa na chama chake, habari ambayo ni mbaya na haikupswa kugusa ngoma za masikio ya Watanzania.
Ikumbukwe kuwa kila chama cha siasa kimesajiliwa, kikitekeleza ilani yake, sera na kanuni walizozikubali wao na kama CHADEMA wamekaa na kutafakari kwa kina wakaona kuwa wana sababu ya msingi ya kukutana na rais wao,iweje wazuiwe kwa masharti ya ajabu na chama kingine cha siasa tu kwa sababu eti ni mwenyekiti wao na ni rais kutoka CCM.
Kwa ukongwe wa CCM hata mara moja hawakupaswa kuvitafutia vyama vingine nafasi ya kukutana na rais kwa sababu inaonyesha wazi havikuwa na hoja ya kutaka kuingia Ikulu kwa sababu za kitaifa kama ombi la CHADEMA lilivyowasilishwa na kukubaliwa.
Kwa maana hiyo utata uliojitokeza kuhusu uanzishwaji wa mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya sio tu kutainufaisha chadema ikukutana na rais la hasha wanachopaswa kukifahamu CCM kuwa CHADEMA hawaendi Ikulu kuonana na rais ili wawe na katiba yao hilo nalo ni upuuzi unaotaka kuzaliwa.
Ikubalike kabisa kuwa ushauri wanaoweza kuutoa viongozi wa chama hicho cha upinzani kwa rais wao kunaweza kuisaidia zaidi serikali ya Kikwete isijiingize kwenye mgogoro wa kisheria kuliko dhana potofu inavyotaka kujengwa na kundi la watu wachache wanaojifanya kuwa ni makada mahiri wa chama hicho wasiokuwa na kashfa za kutakiwa kujivua gamba.
CHADEMA kama chadema waachwe wakutane na rais wao,waeleze kile walichokusudia kukusema na kushauri na nafasi ya rais aliyonayo ni ile ya kuwasikiliza na kupokea ushauri atakaopewa, akiona haumfai aachane nao na kama ataona ushauri huo unafaa aufanyie kazi kwa ajili ya masilahi ya nchi na Watanzania wote.
Hasa kwa kuzingatia kuwa Katiba inayokusudiwa kuandikwa kwa kujali maoni ya wananchi ni katiba ya nchi na si katiba ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na vyama vingine vya siasa vilivyosajiliwa hii katiba inayovuta utashi wa kisheria ni ya nchi hapo ndipo somo linapopaswa kuelekezwa.
Kwa wale Wakristo wenye sheria za kufanya maungamo kwa Mapadre haiwezekani mtu anayetaka kwenda kuungama mambo yake ya siri eti lazima asindikizwe na mtu mwingine asiyehusika na maungamo hayo ya kiimani na hajui nini kitakachoweza kusikilizwa na padri huyo kutoka kwa muumini wake mwenye shida.
CHADEMA wanataka kwenda kufanya maungamo ya kisheria na rais wao,wao ndio wanaojua siri ya kile wanachotaka kwenda kusema, lengo kubwa likielekeza kwenye mwelekeo sahihi wa kitaifa katika kushauri.
Hawaendi huko kuwachongea wana CCM na kumtaka rais awabane mafisadi waliotajwa Mwembe Yanga, hayo sidhani kama ndio hoja ya vigogo wa CCM kuwa na matumbo moto.
Kwa vyovyote suala la mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhiwa na rais mwenyewe na itashangaza kama rais huyo huyo anaweka mipaka isiyokuwa na tija ambayo mwisho wake kunaweza kuzaa vurugu na balaa kama nchi nyingine za Kiafrika wakiwamo majirani zetu wa Kenya walivyoshuhudia vurugu na mauaji pale waliposhindwa kuheshimiana katika hoja za msingi.
Kwa kujali na kutambua mchango wa vyama vya siasa katika kusukuma maendeleo ya nchi,kulinda na kuhamasisha hali ya usalama ipo haja ya rais kujiwekea utaratibu wa kukutana na viongozi wa upinzani kwa muda unaofaa hasa pale migongano ya kimtazamo inapojitokeza, kikubwa utaifa uwekwe mbele kuliko itikadi ya vyama.
Hakuna rais wa CCM,watanzania wanajua kuwa yupo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nchi inayozingatia sheria za mfumo wa vyama vingi vya siasa, Kikwete aachwe afanye kazi zake bila kuingiliwa, amalize awamu yake bila madoa ya ubaguzi wala umwagaji wa damu usiotarajiwa, Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment