CHAMA cha siasa kilicho makini ni kizuri, na uzuri wake haubaki tu ndani ya chama bali utaenea na hata kuvuka mipaka ya chama na wakati mwingine kuviingilia vyama pinzani. Uzuri ni uzuri hauna tafsiri nyingine.
Sasa hivi uzuri wa umakini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umechanua na kinaongelewa kila mahali.
Hapa nataka niuangalie uzuri huo nikiwa nimesimama upande wa chama tawala, CCM ili kuondoa dhana ya kwamba pengine nakipendelea chama hicho kinachoongoza kambi ya upinzani nchini kwa usemi wa kwamba muwamba ngoma huvutia kwake.
Kwa muda mrefu siasa za nchi yetu ilitawaliwa na ukiritimba, kuanzia chama kimoja cha siasa, ukiritimba ndani ya chama hicho kimoja uliosababisha kujitokeza kwa kaulimbiu ya “zidumu fikira za mwenyekiti” kana kwamba wanachama wengine wa chama hicho hawakuwa na fikira za aina yoyote.
Wanachama, makada na viongozi wengine wa chama hicho hawakuwa na fursa ya kutoa fikira zao bali kubaki tu wakizitukuza fikira za mtu mmoja, mwenyekiti.
Hiyo ni fursa iliyopotea ya chama kama taasisi iliyopaswa kuonyesha umakini wa kuzichanganya fikira za watu mbalimbali na kisha na kuibuka na mtazamo wa pamoja ulio imara na endelevu.
Kwahiyo ukiritimba wa mawazo ndani ya CCM uliwalazimisha watu, wanachama, kuyanyamazia mambo hata yale yaliyojionyesha wazi yanaenda kombo na kuipeleka nchi mrama.
Mtu mwenye fikira ambazo pengine zingeweza kuokoa jahazi hasingethubutu kuzitoa na badala yake angeendelea kuzitukuza fikira za mwenyekiti hata kama alikuwa anaiona hitilafu katika fikira hizo.
Katika hali hiyo, kunyanyasana, kukandamizana, kuoneana wivu, kuchongeana, kuhujumiana na kupakana matope yalikuwa ni mambo ya kawaida ndani ya CCM.
Aliyejaribu kupinga hali hiyo angetengwa na hata kufukuzwa ndani ya chama kama njia ya kumshikisha adabu. Na ilibidi mtu ashike adabu kwelikweli kwa vile hapakuwa na mahali pengine pa kukimbilia, chama kilikuwa kimoja.
Tumshukuru Mungu mwenyekiti wa wakati huo, Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere alikuwa ni mtu ambaye kwa kiasi kikubwa alijitosheleza kimaamuzi.
Angekuwa ni mtu wa kuyumba yumba na kutetereka sijui chama na nchi vingekuwa katika hali gani kwa mwenendo huo ambao Waingereza wanasema “one man show”.
Sababu wakati huo mwenyekiti wa CCM alikuwa nao uwezo wa kuubadili mfumo wa chama kadiri alivyotaka uwe bila pingamizi lolote.
Tuseme angeingiwa na pepo na kuamua kuifuta jumuiya yoyote ya chama, mfano Jumuiya ya Vijana (UVCCM), sidhani kama kuna kijana yeyote ambaye angethubutu kuukemea uamuzi huo. Wakati huo watu walikuwa wanamalizana kimyakimya ndani ya chama hicho kama usemi wa siku hizi ulivyo wa kuchinjiana baharini ambako damu haionekani.
Ninachotaka kukionyesha katika makala haya ni jinsi mambo yalivyobadilika. Nidhamu ndani ya CCM inaonekana kuimarika, sio ile nidhamu ya kinafiki wala nidhamu ya woga kama ya wakati ule, ila nidhamu ya kweli ambapo mdogo anamheshimu mkubwa na mkubwa anamheshimu mdogo kwa wote kutendeana haki.
Hali hiyo inaondoa kuhujumiana, kuoneana, kupakana matope na kulifanya suala la kuchinjiana baharini kama njia ya kutoana kafara libaki ni jambo la kusadikika tu ndani ya chama hicho.
Mabadiliko hayo ndani ya CCM, kama yalivyojidhihirisha wakati wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM vilivyoisha juma hili kule Dodoma, hayakuja kama mvua. Nitaeleza baadaye.
Ipo mifano kadhaa ambayo tangu enzi za TANU wanachama walikuwa wakitolewa kafara ili kujenga woga ndani ya chama na kuwafanya wanachama wasiweze kuhoji mambo ya msingi ndani ya chama chao. Na baadaye wakati wa CCM.
Tunamkumbuka aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar alivyotolewa kafara baada ya kuhoji uhalali wa serikali mbili katika Muungano wa Tanzania badala ya serikali tatu, yaani Zanzibar, Tanganyika na Serikali ya Muungano.
Nyerere alimshushua waziri huyo kiongozi akiuliza mtu huyo alijifunzia wapi hesabu ya moja kuongeza moja kwamba jibu lake ni tatu!
Pamoja na kwamba alichokuwa akikisema Waziri Kiongozi lilikuwa ni jambo la msingi, kwa maana ya kuwa na Serikali ya Tanganyika kama ilivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye Serikali ya Muungano, lakini kwa vile jambo hilo lilikuwa nje ya fikira za mwenyekiti ikabidi Waziri huyo Kiongozi atolewe kafara.
Kipindi hicho hicho kafara ikamkumba mzee Aboud Jumbe Mwinyi wakati akiwa rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Makamu wa mwenyekiti wa CCM na makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hizo zote naziita kafara sababu makosa ya wahusika hayakuweza kuthibitishwa kimantiki zaidi ya kwamba walihitilafiana na fikira za mwenyekiti.
Mtu mwingine aliyetolewa kafara kwa mtindo uleule ni Maalim Seif Sharif Hamad, wakati huo naye akiwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.
Baada ya ujio wa vyama vingi vya siasa nguvu za kafara za CCM zimepungua kwa kiasi kikubwa, kutoana kafara kumeanza kuwa kugumu maana wanachama wanajua mahali pa kukimbilia na kuendelea kutoa sauti zao.
Uwepo wa chama makini, CHADEMA, imekuwa tiba kamili na chanjo tosha kwa ugonjwa huo wa kutoana kafara uliokuwa ukiisumbua CCM kwa miaka mingi.
Ikumbukwe mwaka 1995 aliyekuwa anawania nafasi ya kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Karatu, Dk. Willibrod Slaa, naye alitolewa kafara baada ya kushinda kura za maoni lakini akakosa kupata nafasi hiyo baada ya chama kumuona si mwenzao na kupendekeza jina la mtu aliyeshika nafasi ya pili ndiye awe mgombea wa chama hicho jimboni humo.
Slaa alipoona ameenguliwa akaamua kujiunga na CHADEMA ambapo alipata fursa ya kuwania ubunge na alimuangusha huyo kipenzi cha CCM mara mbili, 1995 na 2000 wakati akilishikilia jimbo hilo mara tatu kabla ya kumuachia kamanda mwingine wa CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo yeye aligombea urais.
Kwahiyo tutaona kwamba isingekuwa CHADEMA wapiga kura wa Karatu wangekuwa wanawakilishwa na mbunge asiyekuwa chaguo lao kutokana na ugonjwa wa CCM wa kutoana kafara.
Vivyo hivyo tiba ya CHADEMA ikajitokeza katika jimbo la Bukombe. Profesa Kahigi alionekana si mwenzao baada ya kuwania kura za maoni na kuongoza ndani ya CCM lakini akaenguliwa kwa mtindo wa kafara.
Kahigi akaamua kwenda kwenye chama kinachojali masilahi ya umma bila kuendekeza “umwenzetu” wa wachache, sasa Kahigi naye ni mbunge. Angebaki CCM wapiga kura wa Bukombe wangekuwa na mbunge ambaye si chaguo lao.
Maswa Magharibi nao wakanufaika na tiba ya CHADEMA, baada ya Shibuda kuenguliwa kwa nguvu ya rushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM akaamua naye kukata rufaa CHADEMA, sasa ni mbunge.
Baada ya hapo mtindo wa CCM wa kutoana kafara ukaja kwa staili mpya ya kuvuana magamba. Swali lililopo ni la kwamba tangu lini kobe akavua gamba akabaki mzima? Hicho ni kitendawili ambacho hata kama nikipewa mji bado kitaniwia kigumu kukitegua.
Kwa siku za karibuni imekuwa ikidaiwa kwamba mbunge wa Monduli na aliyekuwa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu (kwa kafara?) Edward Lowassa, ni gamba lililokuwa likitakiwa kuvuliwa kwa nguvu zote ndani ya CCM.
Inaeleweka kuwa Lowassa ndiye aliyekuwa mhimili wa JK, mwenyekiti, kuweza kukikalia kiti cha enzi. Inawezekanaje mtu huyo aonekane gamba, avuliwe na mwenyekiti abaki salama?
Hapo ndipo tukuangalie vizuri kuvuana gamba, ni kweli huko ni kuvuana gamba au kutoana kafara?
Lakini hiyo yote ni kwa sababu kumejitokeza chanjo ya ugonjwa huo wa kutoana kafara, vinginevyo watu wengi wangeishaondoka na maji ndani ya CCM kwa mtindo wa kuchinjiana baharini.
Baada ya chanjo hiyo ya CHADEMA kuonyesha mafanikio vijana wa CCM, UVCCM, kupitia kwenye jumuiya yao wakaja juu wakihoji mambo mbalimbali ambayo huko nyuma yalikuwa hayahojiki.
Mara zikaja tetesi kwamba ulikuwepo mpango wa CCM kuifuta jumuiya hiyo ya vijana, vijana wakachachamaa na baadhi yao kutoa kauli kwamba wanakwenda Dodoma, kwa ajili ya vikao vya NEC na CC vya chama chao, wakiwa wana CCM lakini kuna uwezekano wa kurudi wakiwa CHADEMA.
Baadaye nikasikia mwenyekiti wa CCM, JK, akiwachimba mkwara vijana hao kwamba wasitoe vitisho, kama ni CHADEMA wanaweza kwenda. Lakini kadiri mambo yalivyoenda kule Dodoma tunaweza kuona ni yupi aliyetishika.
Kauli hiyo ya JK ilikuwa ya kinadharia zaidi, nilitaka Kikwete atamke kwamba tangu leo hakuna kinachoitwa Umoja wa Vijana wa CCM ndipo niamini kwamba alikuwa hatishiki na mkwara wa UVCCM. Maana wao walitaka waonyeshwe kitendo ndipo nao watende, vinginevyo imebaki kutishiana nyau.
Kwa vyovyote vile Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimejionyesha kuwa muarobaini wa matatizo ya kisiasa nchini.
Maana kukandamizana, kunyanyasana, kuoneana wivu, kuhujumiana, kusalitiana, kupakana matope na mwisho kutoana kafara, kwa walio waumini wanaamini kwamba hizo ni dalili za ushetani, na shetani ni mtovu wa nidhamu.
Kwa hiyo hali yoyote inayoifanya CCM kuachana na mambo hayo ni lazima tuitaje kama hali ya ukombozi. Na kama hali hiyo imetokana na CHADEMA sidhani kama nitakosea kusema kwamba CHADEMA ni mkombozi wa CCM kutoka kwenye pepo wachafu.

No comments:
Post a Comment