Thursday, December 15, 2011

JK ahudhuria Mkutano wa Maziwa Makuu

RAIS Jakaya Kikwete jana ameungana na viongozi wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka huu wa Umoja huo mjini hapa.

Rais Kikwete na ujumbe wake, waliwasili nchini Uganda jana asubuhi na kwenda moja kwa moja kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili.

Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mkutano huo ni pamoja na Rais Michael Sata wa Zambia ambaye amemaliza muda wake wa kuwa Mwenyekiti wa ICGLR na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, mwenyeji wa mkutano huo na Mwenyekiti mpya wa Umoja huo.

Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Rais Mwai Kibaki wa Kenya na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi.

Nchi nyingine wanachama wa ICGLR zilizowakilishwa na viongozi wa ngazi mbalimbali ni Sudan iliyowakilishwa na Makamu wa Rais, Dk. Alhaj Adam Yusuf, Angola, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Congo Brazzaville na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo jana, viongozi na wawakilishi wa nchi wanachama wa
ICGLR wamejadili suala zima la Ukatili wa Kijinsia na athari zake katika nchi za Maziwa Makuu ambako kumekuwa na aina moja ya vita na mapigano kwa miaka 17 iliyopita.

Ukatili wa Kijinsia katika nchi ambazo zinakabiliwa na mapigano na vita ama zimetoka katika hali hiyo unachukuliwa kuwa ni pamoja na ubakaji, mashambulizi ya kijinsia, kupiga, utekaji nyara, mauaji ya makusudi, utumwa wa kijinsia, ndoa za kulazimishwa na kufanya mapenzi na watoto wadogo.

Leo mkutano huo utajadili masuala mengine yanayohusu Umoja huo ikiwemo hali ya usalama
katika nchi wanachama wa ICGLR na kupokea na kujadili ripoti ya mkutano wa mawaziri wa usalama na ulinzi kuhusu athari za majeshi hasi katika eneo hilo.

Mkutano huo pia utajadili na kutoa uamuzi kuhusu maombi ya nchi za Sudan Kusini kujiunga na ICGLR.

Mkutano huo wa mwaka huu pia utajadili maendeleo yaliyopatikana kutokana na maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano maalumu wa ICGLR uliofanyika Lusaka, Zambia mwaka jana kuhusu mapambano dhidi ya uvunaji na biashara haramu ya maliasili za nchi hizo.

Katika kikao hicho, wakuu hao wa nchi pia watateua Katibu Mtendaji mpya wa ICGLR kutokana na kumalizika kwa kipindi cha uongozi cha Balozi Liberata Mulamula wa Tanzania.

Muhula wa uongozi wa Balozi Mulamula ulimalizika toka mwaka jana wakati wa mkutano wa Lusaka, lakini wakuu wa nchi wanachama wa ICGLR walimwomba Balozi huyo kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja zaidi ili kutoa nafasi kwa nchi wanachama kutafuta watu wanaofaa kujaza nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment