Saturday, December 17, 2011

Kikwete atishwa

WAKATI serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitafakari njia za kukabiliana na siasa za makundi na ugumu wa maisha, viongozi wa dini wamezusha hofu mpya kwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliishutumu serikali ya Rais Kikwete kuwa haikuwa na lengo la kupata maoni ya wadau muhimu kuhusu Muswada wa Mabadiliko ya Katiba mpya.
Kiongozi huyo alisema alishangazwa na hatua ya serikali kumpa muda wa siku nne kutoa maoni yake kuhusiana na muswada huo wa katiba, wakati walijua kuwa alikuwa nje ya nchi kikazi.
Aliweka wazi kuwa yeye ni kiongozi wa taifa, haikuwa busara kwake kupewa muda wa siku nne kujaza fomu ya maoni, huku akihoji iwapo yeye alifanyiwa hivyo, ilikuwaje kwa watu wengine wa kawaida.
Pengo pia alionya kuwa uzembe huo uliofanywa na serikali ndio uliosababisha machafuko katika mataifa mengi kutokana na watawala kuendesha mchakato huo muhimu kizembe na kwa kulinda masilahi yao.
“Lazima tutambue kuwa katiba ni chombo muhimu ambacho kinatuongoza. Rais akichaguliwa lazima aapishwe kwa katiba ili aweze kuilinda. Sasa tumebakiza miaka minne kufika uchaguzi mwingine, kwa kuzembea huku tutajikuta njia panda.
“Najua huko mbele tukikwama wanaweza kusema rais aendelee hadi katiba mpya ikamilike, lakini itabidi aapishwe, sasa ataapa kwa katiba ipi…hii ambayo tunaikataa kuwa haifai ama mpya ambayo itakuwa haijakamilika?” alihoji Kardinali Pengo.
Wachambuzi wa masuala ya jamii wameweka wazi kuwa kauli hiyo ya Pengo imezidisha mtafaruku juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipingwa na wabunge wa CHADEMA, NCCR-Mageuzi na wanaharakati mbalimbali.
Wanaweka wazi kuwa kauli hiyo ni kitisho kwa kiongozi wa nchi ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu wa kujenga umoja na mshikamano wa taifa ambao unaonekana kulega lega.
Wakati Pengo akitoa msimamo huo, Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu hapa nchini, umewataka Waislamu wote nchini kushiriki maandamano ya kudai Mahakama ya Kadhi iliyoahidiwa na serikali ya CCM kwenye ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005.
Msemaji wa umoja huo, Ustaadh Kondo Bungo, alisema maandamano yao yalipata baraka za viongozi wa taasisi mbalimbali za dini ya Kiislamu likiwamo Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Msingi wa hoja ya umoja huo ni kuwa serikali ya CCM iliwahadaa juu ya kuanzisha mahakama hiyo ambayo ni chombo muhimu kwa Waislamu, lakini mpaka sasa haijaanzishwa na katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 CCM imeliondoa jambo hilo.
Wakati viongozi hao wa dini wakionyesha kutoridhika na uwajibikaji wa uongozi uliopo madarakani, wananchi nao wamekuwa wakiulaumu kwa kushindwa kuboresha maisha yao kama ulivyowaahidi mwaka 2005.
Mfumko wa bei hivi sasa umefikia asilimia 19.2 kutoka asilimia 6 mwaka 2005 wakati Rais Kikwete akichukua madaraka kutoka kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Jingine ambalo linamweka Rais Kikwete matatani ni ongezeko la vijana wasio na ajira ambao wamehitimu mafunzo mbalimbali.
Juzi Rais Kikwete akiwa nchini Uganda, alisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu ni bomu linalopaswa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Aliwaeleza viongozi wenzake wa  nchi za Afrika kuwa jambo hilo linahitaji majibu makini ya haraka na hatua kubwa zisizohitaji kucheleweshwa.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na jamii wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa kauli hiyo ya Rais Kikwete inaonyesha wazi anavyotishwa na hali ya mambo ndani ya Tanzania na Bara la Afrika.
Posho za wabunge
Rais Kikwete pia anadaiwa kuwa mpaka sasa hajasaini ongezeko la posho za wabunge licha ya kupelekewa pendekezo hilo na Ofisi ya Bunge baada ya kuzusha mjadala mkubwa katika jamii.
Kutokusaini huko kwa Rais Kikwete, kunaelezwa ni kuhofia kuamsha hasira za wananchi ambao wengi wameonyesha kutokubaliana na ongezeko hilo la posho za wabunge ambazo baadhi ya wabunge wanazipinga.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitangaza kuwa posho ya kikao kwa mbunge imeongezeka kutoka sh 70,000 kwa siku hadi sh 200,000 huku akiweka wazi ongezeko hilo limetokana na ugumu wa maisha unaowakabili wabunge wakiwa mkoani Dodoma.
Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alitaka posho hizo zisilipwe kwasababu maisha magumu yanawakabili wananchi wote na si wabunge pekee.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wameweka wazi kuwa Rais Kikwete hivi sasa ana wakati mgumu wa kushughulikia masuala muhimu ya taifa na chama chake ambacho hivi sasa kimekumbwa na siasa za makundi yanayohasimiana.
Wanadai kuwa siasa za makundi ndani ya chama chake ndizo zinazokwamisha baadhi ya maamuzi ndani ya serikali.
Wameweka wazi kuwa siasa hizo ambazo sasa zinalenga urais wa mwaka 2015 zinaweza kuathiri zaidi mustakabali wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment