Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kimesema, Lowassa aliomba kupewa nafasi ya kuzungumza juzi, lakini Mwenyekiti Rais Kikwete hakumpa nafasi na kumtaka azungumze wakati wa mjadala wa hali ya siasa nchini jana.
Taarifa hizo, zimesema baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, kumaliza kuwasilisha mada kuhusu suala la maadili ndani ya chama, ndipo Lowassa alisimama na kuzungumza.

Pamoja na mambo mengine, katika mada yake, Msekwa alisema masuala yote yanayohusiana na maadili ndani ya chama yashughulikiwe na vikao husika kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.
LOWASSA AZUNGUMZA
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema; “Kwa kipindi cha miezi saba sasa tangu NEC ikutane, Katibu wa Itikadi na Uenezi na viongozi wengine wa chama wamekuwa wakizunguka nchi nzima kunitangaza mimi fisadi kwa kutumia rasilimali za chama.
“Leo hii napongeza ripoti ya mzee Msekwa ya kusisitiza kutumia vikao vya maadili kushughulikia na maswala yote yanayohusika na matendo ya kwenda kinyume na taratibu zetu za chama, lakini leo ninashangaa tunazungumzia kwenda kwenye utartibu huo, wakati mimi nilishaumizwa na ninatoka damu kwa kipindi cha miezi saba,”
“Lakini Mwenyekiti leo hii, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond, wakati makosa yaliyosababisha kashfa ya Richmond yalitokana na makosa ya watendaji walio chini yangu. Mimi niliwajibika kwa ajili ya kulinda heshima ya chama chetu.
AMKUMBUSHA RAIS KIKWETE YALIYOJIRI
“Lakini Mwenyekiti, naamini utakumbuka jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba wa Richmond, nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasikiliza ushauri wa kamati ya makatibu wakuu (Kikwete akatikisa kichwa kukubaliana naye) , mheshimiwa ushauri wa kamati ya makatibu wakuu ndiyo uliopelekea mkataba usivunjwe.
“Pia naomba nikumbushe, nikiwa Waziri wa Maji niliwahi kutuhumiwa kuhusiana na kampuni ya City Water, tena nashukuru Mzee Nimrod Mkono yupo hapa, tukaenda kwenye kesi tukashinda. Sasa katika hili la Richmond kosa langu ni lipi? Je kuwajibika kwa maslahi ya chama changu na ya serikali yangu, utakumbuka ripoti ya Dk. Harrison Mwakyembe wakati anahitimisha Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, alisema kuna aina mbili ya uajibikaji, kwa makosa ya kiongozi mwenyewe na watendaji walioko chini ya kiongozi,
“Dk.Mwakyembe akasema Waziri Mkuu aliyejiuzulu amejiuzulu si kwa makosa yake, bali ni makosa ya watu waliokuwa chini yake (huku akiwa ameshikilia Hansard ya Bunge),”
“Mwenyekiti naomba nikukumbushe kuhusu kashfa zinazohusiana na ‘political perception’, kama si busara za kina Mzee Mkapa mwaka 1997 kule Zanzibar, leo hii usingekuwapo hapo ulipo na ulisema urais ni mipango ya Mungu.
“Unakumbuka kina Mzee Sozigwa jinsi walivyokuja na mafaili kwenye mkutano huo wa NEC kwa ajili ya kukumaliza.
“Hata nilipokutana na Mzee Msekwa pale Dar es Salaam, aliniambia kuna watu wananoa mapanga kwa ajili ya urais wa Lowassa.
“Kibaya zaidi, wanaonitukana ni wana-CCM (Nape, Chilligati na wenzao), lakini hata CHADEMA na wapinzani wengine hawanitukani,” alisema Lowassa.
Baada ya Lowassa kumaliza kuzungumza, Waziri Mkuu mstafuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, alisimama na kuchangia.
Katika mchango wake uliovuta hisia za wajumbe wengi, Sumaye alielekeza swali lake kwa Mwenyekiti, Rais Kikwete.
Katika Swali hilo, Sumaye alitaka kujua wanaotajwa kumtukana Lowassa kwa kipindi chote hicho watafanywa nini. Bila kuchelewa wa kusita, Rais Kikwete alisema; “Watachukuliwa hatua.”
Wajumbe wanyimwa fursa kuchangia:
Baada ya Sumaye kumaliza kuzungumza kulitokea hali ya kutoelewana, ambapo wajumbe wengi wa NEC walitaka kuchangia kutokana na yale aliyozungumza Lowassa.
Miongoni mwao ni mwanasiasa mkongwe na kada mwandamizi wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye pamoja na kunyoosha mkono kiasi cha kutaka kusimama, lakini hakupewa nafasi ya kuzungumza.
Mjumbe mwingine wa NEC na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, baada ya kuona uwezekano wa kuzungumza ni mdogo, aliamua kusema hadharani kuwa, katika kikao kijacho, waasisi wa CCJ wafukuzwe CCM.
Baada ya tafrani hiyo ya wajumbe kutaka kuzungumza na kunyimwa fursa, ndipo Rais Kikwete aliposimama na kusema; “Jamani sasa imetosha, tuachie hapa tulipofikia.
“Kama kuna mtu ana ushahidi kuhusu ufisadi wa Lowassa, basi aulete. Yamekwisha, tukafanye kazi, tujenge chama.”
Wajumbe kutoridhika:
Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, nyuso za baadhi ya wajumbe zilionekana kujawa na huzuni na hali ya kutoridhika.
Baadhi yao walipozungumza na Mtanzania, walisema ilibidi hatua dhidi ya Nape na wenzake zichukuliwe leo (jana), ili suala hilo lifikie kikomo.
“Unajua hapa tumelaza kiporo, ilitakiwa hii leo kieleweke, watu tuondoke hapa kila kitu kikiwa kimemalizika, sasa mambo yamelala mpaka kikao kijacho. Lazima chama kisafishwe,” alisema mmoja wa wajumbe.
No comments:
Post a Comment